Mwanamfalme wa Abu Dhabi amemuonya naibu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel kuhusu itikadi kali miongoni mwa vijana katika misikiti ya Ujerumani. Gabriel, ambaye pia ni waziri wa uchumi, amesema Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahyan amewataka wasilifumbie macho suala hilo kwa kuwa linaathiri watu wote.
Akiwa ziarani katika Falme za Kiarabu, kituo chake cha pili cha ziara yake ya mataifa matatu ya eneo la Ghuba, Gabriel amesema Wajerumani sharti wawe waangalifu nani anayehubiri katika misikiti. Gabriel aidha ameionya Ulaya na mataifa ya Ghuba kuhusu mamilioni ya wakimbizi waliokimbia mizozo nchini Syria na Iraq. Kiongozi huyo wa Ujerumani amewasili Abu Dhabi akitokea Saudi Arabia na anatarajiwa kukamilisha ziara yake kwa kuitembelea Qatar.